Hiki ni kipindi kibaya sana katika mapenzi na mtu anapotokewa na jambo kama hili huathirika sana kisaikolojia kiasi cha kuwa tayari kufanya kitu chochote ili kulipa kisasi. Sio ajabu kusikia mtu fulani kamchinja mkewe, kamuua mumewe, kapigana vikali, kafanya madhara makubwa au kajinyonga baada ya kugundua kuwa mwenzi wake anamsaliti
Kwa kutambua hilo, ndiyo maana nimekuandalia dondoo muhimu ambazo zitakufanya umgundue mapema mpenzi ‘anayekuzunguka’ ili uamue nini cha kufanya kabla mambo hayajazidi kuharibika.
DALILI ZA MTU ANAYEKUSALITI
Kuna dalili nyingi ambazo mtu anayefanya usaliti nje ya uhusiano wake, huzionesha. Kuwa makini kwani sio kila uonapo dalili moja au mbili kati ya hizi, inamaanisha mwenzi wako anakusaliti.
Unapaswa kuchunguza dalili nyingi kwa pamoja ndipo uwe na uhakika kuwa unasalitiwa.
*Kusingizia kazi hata muda wa ziada
Mtu anayekusaliti huanza kuwa na visingio vingi vya kuchelewa kurudi nyumbani. Kila mara atakwambia kuwa alikuwa na kazi za ziada (overtime) na ndio zimemfanya achelewe kurudi nyumbani(Kwa wale ambao ni wafanyakazi). Mara nyingi huu huwa ni uongo kwani uwezekano mkubwa ni kuwa ametoka kukutana na mpenzi wa nje na kazi huwa ni kisingizio anachotumia kuficha uchafu aliokuwa anaufanya.
Inawezekana kabisa mtu akatafuta ushahidi hata wa marafiki zake anaofanya nao kazi kuthibitisha kuwa ni kweli alikuwa kazini wakati si kweli. Kuwa makini sana na watu wa aina hii.
*Kuwahi sana kuondoka anapokwenda kazini asubuhi
Mbinu hii hutumika sana na mtu ambaye ameanzisha uhusiano na kuisaliti ndoa yake na mtu wanayefanya naye kazi katika ofisi moja.
Asubuhi hupenda kuwahi kazini kuliko kawaida ili akifika apate muda wa kuwa na mpenzi wake hata kwa muda mfupi kabla wafanyakazi wengine hawajafika.
Wanaweza pia kuutumia muda huu kwenda sehemu ya faragha na hata kuvunja amri ya sita.
* Kunukia pombe au pafyumu ngeni
Wakati mwingine, mwenza anayekusaliti anaweza akakudanganya kuwa anatoka kazini lakini wakati huohuo akawa ananuka pombe au harufu ya pafyumu ngeni.
Dalili hii huchukuliwa kuwa muhimu sana kwani endapo mwenzi wako ataonesha dalili hii, ni dhahiri kuwa muda mfupi uliopita alikuwa akirusha roho na mtu mwingine. Ni wajibu wa kila mmoja kuwa makini sana na mwenza wake kwani dalili hii inapoonekana, huwa ni hatari sana.
* Kuwa bize na simu muda mwingi
Endapo hukuzoea kumuona mwenzi wako akiwa bize na simu kwa muda mrefu, halafu ikatokea anaanza kuonesha mabadiliko ya haraka, akiutumia muda mwingi kusoma na kuandika sms kwenye simu yake, basi kuna uwezekano mkubwa akawa ameanza kukusaliti.
Inawezekana pia kuwa anapokuwa mbali na wewe, unapompigia simu yake inakuwa bize muda mwingi, huku akiwa hakwambii moja kwa moja huwa anazungumza na nani. Hata anapozungumza na wewe, akili yake huwa iko mbali.
* Kukosa utulivu anapokuwa na wewe
Mwenzi ambaye ameanza kukusaliti, huwa na kawaida ya kukosa kabisa utulivu anapokuwa na wewe. Kama mpo naye ndani basi utaona akijikanyaga mara kwa mara, akidondosha vitu na kuwa na papara zisizoelezeka.
Hii hutokea kwa sababu nafsini mwake huwa anahukumiwa kwa kitendo anachokufanyia, hivyo hujaribu kuzificha hisia zake za ndani, lakini badala ya kuzificha ndiyo huzidi kuzionesha. Pia huwa ni kwa sababu anapokuwa na wewe, akili yake huwa inamuwaza mtu mwingine tofauti kwa hiyo anakuwepo kimwili lakini kiakili anakuwa mbali sana, hivyo umakini hupungua sana.
*Kuondoka nyumbani kwa kuzira mnapogombana
Wenzi wengi hulalamika kuwa wenzi wao wanapoanza kuonesha mabadiliko ya kitabia, inapotokea wakakwazana wakiwa ndani ya nyumba hata kwa jambo ambalo ni dogo, mmoja hujifanya kukasirika sana na kuondoka nyumbani bila kueleza anapokwenda, na anaporudi huwa amebadilika kabisa.
Uwezekano mkubwa ni kwamba mnapogombana, mwenzi wako anaweza kuwa anaitumia nafasi hiyo kikamilifu kwa kukutana na mpenzi wa nje kwa lengo la kujiliwaza.
*Kuanza kupendeza sana kimavazi anapotaka kutoka
Inaelezwa kuwa unapoona mwenzi wako akibadilika ghafla kitabia na kupenda kujiremba sana, kujipodoa na kuvaa nguo zinazomzidishia mvuto kuliko kawaida anapokuwa anataka kutoka, yawezekana anayafanya yote hayo kwa ajili ya kumfurahisha mpenzi wake mpya.
Unapaswa kuwa makini sana unapoona mabadiliko kama haya. Pia utamuona akianza kubadili aina ya mavazi aliyokuwa akipendelea kuyavaa, na zaidi atakuwa akipendelea mavazi yanayomfanya aonekane kijana.
*Kubadili marafiki ghafla
Unapogundua kuwa mwenzi wako amebadilisha marafiki na kuanza kushirikiana na watu wanaotia hofu, basi elewa kuna jambo nyuma ya pazia.
Unaweza kuona mwenzi wako akianza kuwa na uhusiano wa karibu na watu waliomzidi sana umri au ambao ni wadogo sana kuliko yeye.
Urafiki wa aina hii huwa ni kwa sababu kuna siri wanazofichiana au kuna mambo wanayoyafahamu wenyewe na hawapendi mtu mwingine afahamu.
*Kushindwa kupokea simu anapokuwa na wewe
Wengi wamekuwa wakilalamikia sana tabia hii, ambapo wenzi wao hushindwa kupokea simu wanapokuwa nao. Unakuta simu inaita halafu mwenzio anainuka na kwenda kupokelea nje